USIKATE TAMAA WEWE NI MSHINDI

Recent News

Monday, October 29, 2018

Wafanyabiashara wakatazwa kukopesha wakulima


Serikali wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, imepiga marufuku wafanyabiashara kuwakopesha fedha wakulima wa mpunga kwa ajili ya kuendesha kilimo na badala yake imewataka wakulima hao kukopa katika taasisi za fedha zinazotambuliwa kisheria.

Marufuku hiyo ilipigwa juzi na Mkuu wa Wilaya hiyo, Reuben Mfune, wakati wa kikao cha wadau wa kilimo wilayani humo na kusema wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwanyonya wakulima kwa kuwakopesha fedha kwa riba kubwa.

Aidha, alisema baadhi ya wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwakopesha wakulima kwa makubaliano ya kulipwa mpunga baada ya mavuno na kwamba mtindo huo pia unawanyonya wakulima kwa kuwa wanachukua mpunga mwingi.

Hata hivyo, Mfune alisema mikopo hiyo ambayo siyo rasmi imekuwa ikisababisha upotevu wa mapato ya serikali kwa kuwa hailipiwi kodi ya serikali.

"Kwa muda mrefu wakulima wananyonywa na hawa wafanyabiashara, sasa kuanzia msimu huu sitaki kusikia mtu anakopesha fedha na atakayepatikana tutamshughulikia kwa mujibu wa sheria," alisema Mfune.

Aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano kwa serikali kwa kutoa taarifa za mtu yeyote watakayemuona anafanya shughuli hiyo haramu ya kuwakopesha wakulima.

Wenyeviti wa Skimu za Umwagiliaji wilayani humo, walikiri kuwapo kwa wafanyabiashara wanaowakopesha wakulima fedha na kwamba mikopo hiyo ambayo makubaliano inakuwa ni kulipana baada ya mavuno.

Mwenyekiti wa Skimu ya umwagiliaji ya Igomelo wilayani humo, Nelson Msemwa, alisema kitendo hicho kinaathiri maendeleo ya wakulima na kuishukuru serikali kwa kuliona tatizo hilo na kulikemea.

"Hili limekuwa ni tatizo kwa muda mrefu katika wilaya yetu, wakulima wanakuwa kama vile wanawafanyia kazi matajiri maana hakuna ambacho huwa mkulima ananufaika zaidi ya matajiri hao, tunashukuru Mkuu wa Wilaya kwa uamuzi wako," alisema Msemwa.

Hata hivyo, aliiomba serikali kuwasaidia wakulima kwa kuweka mazingira rafiki kwenye taasisi za kifedha ili wengi wakakope huko badala ya kuendelea kuwakimbilia hao wanyonyaji akidai kuwa benki nyingi hazina matawi vijijini.

Kwa upande wake Mtafiti kutoka katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Dakawa ya mkoani Morogoro, Dk. Charles Chuwa, alisema katika miaka ya hivi karibuni mavuno ya mpunga yamepungua maeneo mengi nchini.

Alisema wakulima wengi hufanya kazi kwa mazoea ikiwamo kutozingatia matumizi sahihi ya mbolea kwenye mashamba yao na badala yake kuendelea kulima kwa kutumia mbinu za kienyeji.
Share:

0 comments:

Post a Comment

'; (function() { var dsq = document.createElement('script'); dsq.type = 'text/javascript'; dsq.async = true; dsq.src = '//' + disqus_shortname + '.disqus.com/embed.js'; (document.getElementsByTagName('head')[0] || document.getElementsByTagName('body')[0]).appendChild(dsq); })();

Author Details

Ut wisi enim ad minim veniam, quis nostrud exerci tation ullamcorper suscipit lobortis nisl ut aliquip ex ea commodo consequat. Duis autem vel eum iriure dolor in hendrerit in vulputate velit esse molestie consequat.

Followers

Search This Blog

Support

SUBSCRIBE OUR CHANEL